HISTORIA YA CASFETA
UTANGULIZI
CASFETA ni Jumuiya ya wanafunzi
mabalozi wa Kristo Tanzania, kama jumuiya CASFETA imekuwa na malengo
tangu kuanzishwa kwake. CASFETA ni hitaji la wanafunzi walioko
mashuleni na vyuoni kumuabudu Mungu kulingana na imani ya
kipentekoste. CASFETA imekuwa na malengo ya kuwaunganisha wanafunzi
wote wenye imani ya kipentekoste mashuleni mwetu na pia kuwaleta kwa
Yesu wanafunzi wasiookoka.
Kupitia CASFETA wanafunzi wanwezeshwa
kumtumikia Mungu wawapo mashuleni, hii ni kutimiza wajibu wetu kama
wakristo na pia kuwa na fursa ya kutumia vipawa ambavyo Bwana
ameviweka ndani ya wanafunzi katika utumishi katika nchi yetu ngazi
ya shule na vyuo na mwisho katika ujenzi wa Taifa letu.
Kupitia CASFETA wanafunzi waliookoka
mashuleni wanawajibu wa kupiga vita matendo yote maovu yanayoharibu
jamii kama vile ulevi, utumiaji wa madawa ya kulevya, maambukizi ya
magonjwa ya zinaa kama vile UKIMWI.
Mkazo katika masomo ni jukumu la kila
mwana CASFETA awapo shuleni au chuoni alimradi utumishi wetu uweze
kuthibitishwa. Wana CASFETA wana wajibu wa kusaidiana kimasomo kila
inapobidi ilikuweza kutimiza malengo ya kumtumikia Mungu shuleni au
chuoni.
CASFETA ni chombo ambacho kinaandaa
watumishi wazuri wa sasa na wa siku za usoni kwa hiyo ni wajibu wa
kila mpentekoste hasa wale waliookoka mashuleni na vyuoni kuhakikisha
kuwa chombo hiki kinalindwa , kinatunzwa na kinaelezwa ilikuweza
kutimiza makusudi yake sawa na mpango wa Mungu katika nchi yetu, pia
na kwa wale wasio mashuleni wanawajibu wa kukipeleka chombo hiki
katika sehemu ambazo bado hakijafika.
Kwa kuwa shule na vyuo vinaongezeka
katika nchi yetu,kila mwaka tunakila sababu ya kumshukuru Mungu kwa
hilo na kuwajibika kupeleka CASFETA katika shule hizo na vyuo hivyo.
Namna ambavyo CASFETA inaweza
kuanzishwa katika shule au chuo ambapo hakuna huduma hii ni kama
ifuatavyo;-
Endapo kuna wanafunzi wa kipentekoste
katika shule au chuo na hitaji lipo la kuwa na CASFETA katika
chuo au shule husika mawasiliano yafanywe kati ya wanafunzi na
uongozi wa CASFETA wa Wilaya au Mkoa uongozi huo uweze
kuwasiliana na mkuu wa shule au chuo husika.
Baada ya uongozi wa Wilaya au Mkoa
kukamilisha taratibu zote itakazopewa na shule au chuo husika ndipo
shughuli za kuanzishwa tawi zinaweza kuendelea katika ngazi ya
wanafunzi wenyewe.
Mafanikio ya CASFETA yanatokana
na ushirikiano kati ya wanafunzi katika shule au chuo na makanisa ya
kipentekoste yaliyo jirani CASFETA itaweza kukua na kuendelea katika
utumishi kwa wanafunzi, walimu, washirika na wachungaji wa makanisa
ya kipentekoste kuwa na juhudi ya kazi ya Mungu mashuleni.
MAKUSUDI/MADHUMUNI YA
USHIRIKA HUU.
- Kuwawezesha wanafunzi kumwabudu Mungu kulingana na imani yao ya kipentekoste.
- Kuwaunganisha wanafunzi wote wenye imani ya kipentekoste nchini Tanzania waliookoka (watakaookoka)
- Kuwahamasisha wanafunzi wawe na moyo wa kusaidiana kiroho, kimasomo na kijamii
- Kuwahamasisha wanafunzi wa kipentekoste wajue wajibu wao katika kumtumikia Mungu.
- Kuwafundisha wanafunzi maadili ya kikristo kupiga vita matendo yote yanayoharibu jamii kama vile zinaa na (magonjwa yake kama vile UKIMWI) Utoaji wa mimba, Ulevi, Utumiaji wa madawa ya kulevya, Ubakaji, pamoja na matendo mengine maovu.
- Kuwahimiza wanafunzi wawe na bidii katika masomo yao.
- Kuwasaidia wanaushirika wa CASFETA kielimu kila inapowezekana.
- Kujenga tabia miongoni mwa wanafunzi ya kulipenda na kulitumikia Taifa lao la Tanzania kwa uadilifu.
JINA LA UMOJA HUU NI;
“THE CHRIST’S AMBASSADOR STUDENT FELLOWSHIP TANZANIA” kwa
kifupi ‘CASFETA’
LUGHA
Lugha ya mawasiliano katika umoja huu
ni Kiswahili au kiingereza.
AINA YA USHIRIKA
CASFETA ni ushirika wa wanafunzi wa
aina ya kipentekoste ambao umedhaminiwa na kanisa la Tanzania
Assemblies of God (T.A.G)
Reg.S06246.1981.
CASFETA inaendesha shughuli zake katika
mfumo wa kipentekoste.
NEMBO
1). Nembo ya ushirika huu ni msalaba,
Biblia na kofia na shahada/stahada kama inavyoonekana katika jalada
la mwongozo.
2). Andiko la msingi la ushirika huu ni
methali 1:7 ambalo linasema “kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa
bali wapumbavu hudharau hekima na adabu”
Rangi ya ushirika itakuwa ni nyekundu
na nyeupe
A).Nyekundu - Damu ya Yesu itutakasayo.
B). Nyeupe – Maisha safi ya
utakatifu.